Wednesday, January 15, 2014

ACT-TANZANIA KUISAMBARATISHA CHADEMA

CHAMA kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania), ambacho tayari kimeshapata usajili wa muda kinatajwa kuwa ndio tishio la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kuundwa na idadi kubwa ya vigogo wa chama hicho ambacho kwa sasa kimo ndani ya mgogoro mzito na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wao,
Zitto Kabwe.

Taarifa za uhakika zilitufikia kutoka
kwa mmoja wa watu watakaokiongoza chama hicho kipya, kimebainisha kuwa idadi kubwa ya wanachama wa Chadema wanaoheshimika na kukubalika ndani na nje ya chama wamekubali
kwa hiyari zao kuwa ndani ya ACT-Tanzania na kwamba wanasubiri muda ufike ili wajiunge rasmi.

Hatua hiyo imeonesha dalili za wazi za kukimaliza Chadema na kwamba huenda chama hicho kikafika mwaka 2015 kikiwa mahututi kutokana na kuondokewa na wanachama wake wote wenye mvuto.

Mtoa taarifa wetu ameliambia MTANZANIA Jumatano kwamba ACT-Tanzania tayari kina usajili wa muda mkononi na kwamba kinachofanyika sasa ni kuzunguka kwenye mikoa 10 ili kukusanya wanachama 200 watakaokiwezesha kupata usajili wa kudumu.

Lengo la kufanya ziara hizo ni kuhakikishna chama hicho kinatimiza masharti ya usajili ili
kumpa nafasi Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kufanya ukaguzi kabla hakijaendeleza harakati zake.

Taarifa za uhakika zimebainisha kuwa safu ya uongozi wa chama hicho itaundwa na idadi kubwa ya wanachama kutoka Chadema, ambapo Samson Mwigamba anatajwa kuwa Katibu Mkuu, huku Zitto Kabwe akipewa nafasi
ya kuwa Mwenyekiti wakisaidiwa kwa karibu na wanachama mahiri na wasomi kutoka Chadema.

Amesema Zitto atajiunga na chama hicho mara baada ya Bunge la Katiba kumalizika, ambapo kama atavuliwa uanachama atakuwa tayari kujiunga na chama hicho.

Imebainishwa kuwa mkakati wa chama hicho ni kuhakikisha kinakuwa mbadala wa Chadema na
kwamba dhamira yao kubwa ni kuhakikisha wanaendesha siasa zao kwa kutumia demokrasia ya kweli na hawako tayari kukifanya chama hicho kuwa cha watu wachache.

“ACT-Tanzania kitakuwa chama cha wote na ndio maana tutakuwa na wanachama kutoka kila mkoa na tutakuwa tayari kupomkea mwanachama kutoka chama chochote cha siasa, hatuwalengi waliofukuzwa, sisi tunalenga
wanasiasa wote wenye uwezo wa kuendesha siasa safi,”alisema mtoa habari wetu.

Aidha chama hicho katika kujiimarisha hakina mpango wa kuwania urais kwenye uchaguzi
Mkuu ujao na kwamba nia na malengo yao ni kuwa na idadi kubwa ya wabunge na madiwani,
ambapo wanaangalia kama mikakati yao itafanikiwa mwaka huu, watashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Tuna uhakika wa kuchukua majimbo mengi na moja ya majimbo hayo ni lile la Kigoma
Kaskazini, Arusha Mjini na Iringa Mjini, tunauhakika wa kufanya maajabu, tuache muda ufike,”aliongeza.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu alibainisha kuwa chama hicho kwa sasa kipo chini ya vijana wawili na mmoja kati yao ni Leopold Mahona
ambaye aliwahi kugombea ubunge katika Jimbo la Igunga mwaka 2010 kwa tiketi ya Chama cha Wananchi CUF na baadaye kugombea tena
katika uchaguzi mdogo katika jimbo hilo mwaka 2011.

“Mahona akiwa na kijana mwenzake kutoka Zanzibar walianzisha chama hicho kwa nia ya nchi kuwa na chama chenye siasa safi yenye uwazi, bila shaka nia hiyo itafanikiwa,”aliongeza.

Mahona alitafutwa kupitia simu yake ya kiganjani ili kuzungumzia chama hicho, hata hivyo alishangazwa na mwandishi wa habari hii kuwa na taarifa hizo.

Mshangao huo ulimfanya ashindwe kukubali ama kukataa juu ya uwepo wa chama hicho na kumtaka mwandishi wetu kuacha muda useme.

“Kwanza wewe hiyo habari umepata wapi… ‘I have no comment’ tuache muda utasema, lakini ni vema ukawauliza zaidi hao waliokwambia,”alisema Mahona kwa kifupi.

Kuhusu kujua uwepo wa taarifa za kuanzishwakwa chama hicho, alipatwa na kigugumizi zaidi
kwa kujibu kuwa “aaaaaaaa…sijui…
sijui…,”alisema

Alipotafutwa Mwigamba ili kuzungumzia taarifa hizo, ambapo alicheka na kusema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa na kwamba ni vema likaachwa kwani
kwa upande wake bado hajaamua nini cha kufanya kwenye siasa.
“Natafakari, bado sijajua
nifanyeje, hili tuliache kwanza,”alisema kwa
kifupi.

Alipotafutwa Zitto ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, hakuweza kupatikana.

Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo walivuliwa uanachama Januari 5 mwaka huu na Kamati Kuu ya Chadema.

Zitto alishindwa kuvuliwa uanachama kutokana na kukimbilia Mahakamani kuweka zuio kwa Kaamati Kuu kutoujadili uanachama wake.

Dk. Kitila, Mwigamba na Zitto wanashutumiwa na uongozi wa juu wa Chadema kuwa ni wasaliti na kwamba wameandaa waraka wa siri
wenye lengo la kufanya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama hiyo hali iliyoibua mgogoro
mzito.

Mchimba riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score