Friday, January 17, 2014

Maajabu Ya 2014: Wezi Wavamia Gereza Na Kuiba Mbuzi 43

MAAFISA wa ulinzi katika gereza la Kilifi mjini usiku wa alhamisi walilazimika kufyatua risasi
hewani baada ya wezi kuvamia gereza hilo na kuiba mbuzi 43 wanaofugwa katika gereza hilo.
Kiza hicho cha kufyatua risasi hewani kilileta wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi wa Kilifi
ambao walidhania kulikuwa na jambo hatari zaidi mjini Kilifi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, afisa mkuu wa polisi mjini Kilifi Justine Nyaga alisema wezi hao
ambao idadi yao haikubainika walivamia jela hilo mwendo wa saa
saba usiku na kuanza kuiba mbuzi hao.
Hata hivyo afisa wa magereza ambaye alikuwa kazini alipuliza kipenga cha kuashiria hatari ndipo wengine wakaanza kufyatua risasi hewani kuwakimbiza wezi hao.
“Ulikuwa ni mwendo wa saa saba usiku ambapo wakora ambao walikuwa ni zaidi ya watatu walipofika katika gereza hilo na kupenya kabla ya kuanza kuwatorosha mbuzi hao mali ya
gereza hilo.
Hata hivyo afisa wa magereza ambaye alikuwa kazini aliwaona na akapiga kipenga cha kuashiria hatari. Ni hapo ambapo maafisa wengine walianza kufyatua risasi hewani na wezi wakatoroka,” akasema.
Aidha Nyaga alisema kuwa mbuzi wote 43 walipatikana huku wezi hao wakitoroka na bado polisi wanawasaka.
“Tumepata mbuzi wote. Walikuwa hawajafika mbali na baada ya maafisa wa gereza kuanza kufyatua risasi, wezi walitoroka na kuacha mbuzi hao karibu na jela hiyo.Wote 43 ambaowalikuwa wamelengwa na wezi hao wamepatikana,” akasema.
Wakati huo huo, Nyaga alisema kuwa wanachunguza ripoti kwamba kuna soko la siri mjini Kilifi ambapo mbuzi wanaoibwa huuzwa na kisha kusafirishwa hadi maeneo mengine
kuchinjwa ama kuuzwa.
Soko
“Tunajaribu kuchunguza kwa kina tuone hasa jambo hili lilikuwa vipi. Tuko na habari kwamba kuna soko la siri ambapo mbuzi na mifugo
wengine wanaoibwa hupelekwa hapo na kisha baadaye wanunuzi wa siri hufika na kufanya biashara hapo.
Tunataka kuwahakikishia wakazi
wa Kilifi kwamba tuko macho kukabiliana na wezi na wakora ambao watakuwa wakihangaisha
raia wema katika eneo hili,”akasema.
Kufyatuliwa huko kwa risasi na maafisa wa magereza kulizua hofu kuu miongoni mwa wakazi wa Kilifi ambao walidhani maafisa wa polisi walikuwa wakikabiliana na majambazi hatari.
Kulingana na Karisa Charo ambaye ni mwendeshaji piki piki ya boda boda alilazimika 'kutoroka mbio na kujificha baada ya milio hiyo
ya risasi kusikika mfululizo.
“Mazee, nilishutka sana. Mimi hukesha nikiendesha biashara hii lakini punde tu baada
ya mlio wa kwanza, kisha ikafuata mengine ghafla, hata nilivyopeleka pikipiki sikufahamu, nilijikuta eneo la mbali ghafla. Ilikuwa inatisha
sana,” akasema.
Maafisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi pia kubaini kiini cha wizi huo katika gereza hilo ambalo daima huwa na ulinzi mkali.
Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score