Thursday, January 16, 2014

Msigwa wa (CHADEMA) Kunyaganywa Jimbo La Iringa Mjini

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kimetangaza mpango mkakati wa kulikomboa Jimbo la Uchaguzi la Iringa Mjini.

Mpango huo ulitangazwa katika
mkutano mkubwa, uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Mwembetogwa mjini hapa.

Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na
Mchungaji Peter Msigwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyechaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Kwa kupitia mkakati huo, CCM itakuwa ikifanya mikutano ya mara kwa mara katika kata zote 16 za Manispaa ya Iringa.

Lengo la hatua hiyo ni kupokea kero za wananchi na kutoa ufafanuzi wa shughuli za maendeleo, zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na serikali yao.

Mpango huo umebuniwa na Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa,Hassana Mtenga ambaye kabla ya kuhamishiwa mjini hapa, alikuwa Katibu wa chama hicho Wilaya ya
Hai mkoani Kilimanjaro.

Mtenga ambaye pia ni Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, alimuagiza Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi wa
CCM kuhakikisha fedha zinazotengwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake, zinatolewa kwa wakati.

“Wakati mkitoa fedha hizo kwa makundi hayo, wananchi msisahau kumuuliza Mbunge wenu anazitumia vipi fedha za
Mfuko wa Jimbo zinazotolewa na serikali ya CCM kwa ajili ya maendeleo yenu,” alisema
Mtenga huku akishangiliwa.

Agizo lingine alilolitoa kwa madiwani wa Manispaa hiyo, linawataka kuunda Kamati
ya Madiwani wa CCM, watakaofanya kazi ya
kukusanya kero zote zinazowakabili
wananchi wakiwemo vijana wa jimbo hilo.

“Tunaanza kumshughulikia Msigwa kuanzia sasa, hatutalala, tutapita kila mahali na kuwaeleza wananchi kazi zilizofanywa na serikali ya CCM, lakini tutachukua kero zao na kuziingiza katika mipango ya serikali
yetu; lengo la CCM ni kupeleka maendeleo kwa wananchi miaka yote tangu ianze kutawala nchi.

“Nakutahadharisha Mchungaji Msigwa, kiinua mgongo utakachopata kitumie na
familia yako, usirudi Jimbo la Iringa Mjini kwa sababu utapata hasara kubwa,” alisema.

Aliwaomba vijana waache kudandia maneno ya Mbunge huyo, bila kuyatafakari kwa kina kwa sababu yamekuwa yakipingana na mambo anayofanya.

Akinukuu taarifa iliyotolewa na Mchungaji Msigwa katika mkutano wake alioufanya hivi karibuni mjini Iringa, Mtenga alisema;
“anawadanganya wananchi wa Iringa kwamba amepata fedha za kujenga uwanja wa Ndege wa Nduli na mradi wa maji katika Kata ya Nduli, wakati yeye na wabunge
wote wa Chadema huwa wanapinga bajeti ya serikali kila mwaka.

“Muulizeni anapata wapi fedha kwa ajili ya maendeleo ya Iringa, wakati kila awapo bungeni huwa anapinga bajeti ya serikali, ambayo ndio msingi mkuu wa maendeleo
anayoyazungumza,” alisema.

Jumla ya maswali 25 yaliulizwa na kujibiwa na madiwani mbalimbali, waliohudhuria mkutano huo, mojawapo likiwa ni kuhusu
msimamo wa CCM baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupandisha bei ya umeme.

Mtenga alisema wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu, wakati serikali ikiendelea
kujipanga kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo kupitia miradi mbalimbali inayoanzishwa, ikiwemo ya gesi asilia.

Wengine waliopata fursa ya kuhutubia mkutano huo ni vijana waliojitoa Chadema na kujiunga CCM, Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM Taifa (NEC), Mahamudu
Madenge, Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM Ritta Kabati, Mwenyekiti wa CCM
Manispaa ya Iringa Abei Kiponza, Meya wa Manispaa ya Iringa na madiwani.

Habari Leo (Chimbuko)
Mchimba riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score