Dar es salaam, Tanzania
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina
Mohamed, ametetea mkutano wa Kenya na
Rwanda na Uganda mjini Kigali mwezi uliopita
bila ya wanachama wenzao wa Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki (EAC) Burundi na Tanzania ,
liliripoti gazeti la Daily News la Tanzania siku ya
Jumatatu (tarehe 11 Novemba).
Mohamed, aliyekwenda jijini Dar es Salaam siku
ya Jumapili, alisema mkutano huo ulijadili
masuala yenye maslahi ya moja kwa moja ya
pande hizo mbili na kulenga kwenye maeneo
ambayo yanaweza kuwa yaliachwa kwenye
mkutano wa kikanda wa EAC.
Mkutano huo ulijadili ukosefu wa ufanisi wa
bandari ya Mombasa ambao ulikuwa ukiziathiri
Rwanda na Uganda ambazo hazina bahari,
alisema Mohamed, akiongeza kwamba ulifanyika
kwa mujibu wa sheria za jumuiya ya EAC na
hauakisi kutengwa kokote kwa wanachama
wengine.
Pia aliisifu hotuba ya hivi karibuni ya Rais Jakaya
Kikwete wa Tanzania ambayo ilizikosoa Kenya,
Rwanda na Uganda kwa "kujibagua zenyewe "
kutoka wanachama wengine wa EAC kwa
kuunda "muungano wa wenye dhamira" na
kusaini makubaliano kati yao.
Alisema Kenya itahakikisha inaimarisha
mafungamano na wanachama wote wa EAC
katika siku zijazo. "Tutafanya kila tuwezalo
kuhakikisha kwamba EAC inaimarika chini ya
mataifa matano wanachama wa EAC na kuleta
maendeleo kwa watu wote," alisema Mohamed.
By Mchimba Riziki
0 maoni:
Post a Comment