Friday, December 5, 2014

2017 Haitafika Bila Taji "Arsen Wenger" Anena

Kocha wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger ana imani anaweza kuongoza vijana wake kunyakua taji la ligi kuu kabla ya kandarasi yake kuisha mwishoni wa msimu wa 2016/17.

Arsen Wenger

Imani yake ya msimu huu ilipigwa jeki hata zaidi na ushindi wao mwembamba wa 1-0 dhidi ya Southampton Jumatano usiku na hivyo kuzidi kumpa moyo licha ya kuwa wangali katika nafasi ya sita kwa alama 23, ikiwa ni pointi 16 nyuma ya viongozi Chelsea.

Timu hiyo imeandikisha mwanzo wao mbaya zaidi katika ligi ya EPL tangu 1982 na wamejikuta nyuma mno kwa pengo hilo kubwa la alama ikilinganishwa na muhula uliopita ambapo hadi kufikia wakati huu walikuwa uongozini kabla ya kufifia kufikia mwisho wa kampeni na kunusurika kwa kumaliza wa nne.
“Kuna ushindani mkubwa Uingereza na Chelsea wameanza vyema, hilo tunakubali. Itakuwa vigumu kuwafikia lakini kila mmoja atapigania kuwalaza sisi pia tukiwemo. Huwezi kusema kuwa harakati za kuwania taji zimekwisha baada ya mechi 14 pekee tulizocheza hadi kufikia sasa,” Wenger akasema.
“Hatukuanza vyema msimu huu ila usisahau kwamba hatukuwa na kikosi chote pamoja tangu musimu kuanza kwani ulifuatia Kombe la Dunia. Ni lazima tupambane  ili kurudia uwaniaji wa taji kwa haraka katika kila mechi,” akajitetea.

Licha ya yote, Wenger anaonekana kuwa kakalia kuti kavu baada ya mashabiki kuanza kumshurutisha aondoke kama ilivyoshuhudiwa wikendi iliyopita kwenye ushindi wao wa 1-0 dhidi ya West Brom.

Kesi Ya Uhuru Kenyatta Imetupiliwa Mbali.

Wakenya Wakionyesha Furaha Baada Ya Uhuru Kufutiwa Kesi
Habari zilizofika mapema hivi leo zinasema mwendesha mashitaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC Fatou Bensouda, ametupilia mbali mashitaka dhidi ya Rais wa Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Mapema wiki hii mahakama ya kimataifa ya uhalifu  ICC ilimpa wiki moja mwendesha mashitaka huyo kuongeza  kasi ya uchunguzi ama kuyatupilia mbali mashitaka dhidi ya Rais Kenyatta.
Mh.Uhuru Kenyatta
Kesi hiyo iliahirishwa mara kadhaa na mahakama hiyo ya The Hague, na Jumatano ilisema kwamba kuchelewa zaidi kungeweza kuwa kinyume na maslahi ya haki katika mazingira yaliyokuwepo.
Rais Kenyatta alikabiliwa na mashitaka dhidi ya ubinadamu akishutumiwa kupanga ghasia za  baada ya uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2007 na mapema 2008. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu 1,100 huko Kenya na kuwakosesha makazi wengine zaidi ya nusu milioni.
Rais Kenyatta mara kadhaa amesema yeye hana hatia.

Saturday, September 6, 2014

Mwanaume Mmoja Afunga Ndoa Na Maiti..... Ni Wapi Fuatana Nami Mchimba Riziki Nikujuze


MWANAMUME alishangaza familia yake, marafiki na wanakijiji alipoamua 'kufunga’ ndoa na marehemu mkewe katika kijiji cha Kadzinuni, tarafa ya Kikambala, Kaunti ya Kilifi wakati wa mazishi yake.

Kiti Mwangudza Chilango aliamua kutimiza ahadi aliyokuwa amempatia mkewe miaka michache iliyopita kwamba wawili hao wangefunga ndoa rasmi.

Akiwa amevalia suti, Bw Chilango alisimama kando ya jeneza la mkewe akiwa pamoja na msafara wa wasimamizi wake sawa na jinsi inavyofanyika wakati wa harusi.

Pia kulikuwepo na keki ambayo aliikata na kisha ikagawanywa kwa waombolezaji kabla ya mwili kuzikwa.

Kulingana na rafiki wa karibu wa marehemu, Bi Mbeyu Mbura, Bw Chilango alikuwa amemuoa kwa kitamaduni lakini mkewe alikuwa akishinikiza wafanye harusi kanisani.

Bi Mbeyu alifichua kuwa marehemu ambaye alikuwa akiugua ugonjwa usiojulikana alikuwa amemtaka mumewe aape kuwa atamheshimu kwa kumfanyia harusi awe hai ama akiwa amekufa, na ndio sababu mumewe hakuwa na namna nyingine ila kutimiza ahadi hiyo.

“Tunahofia kuwa kitu kibaya huenda kikatokea kwa mumewe ama familia ikiwa ombi la marehemu halitatimizwa. Mumewe anaweza hata kufa,” alieleza Bi Mbeyu.

Mzee wa kijiji Kai Mwandeje alisema kuwa hakuna jambo kama hilo limewahi kutokea eneo hilo na kusema kuwa kitendo hicho huenda kikaleta matatizo mengine baadaye ikiwa mume ataamua kuwa anataka kuoa tena katika siku za usoni.

“Kuvalia mavazi ya harusi kunamaanisha kuwa roho ya mume tayari imeunganishwa na ya marehemu. Itakuwa vigumu kuoa tena isipokuwa kama ahadi hiyo itavunjwa,” alisema Bw Kai.

Thursday, July 31, 2014

Gaza On Fire: Ghaza Katika Lindi La Moto Na Damu

Gaza On Fire
Utawala wa Kizayuni wa Israel leo umeendelea kudhihirisha sura yake halisi ya ugaidi, ukatili na unyama baada ya kushambulia shule nyingine ya Umoja wa Mataifa katika eneo la Jabali huko katika Ukanda wa Ghaza na kuua raia wasiopungua 20 wa Kipalestina.

 Familia nyingi za Kipalestina zimekimbilia katika shule hizo za Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kulinda maisha yao mbele ya mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na jeshi la Israel dhidi ya watu wa Ghaza. Shule hiyo ni ya tatu ya Umoja wa Mataifa kushambuliwa na jeshi la Israel katika mashambulizi ya sasa ya utawala huo haramu katika Ukanda wa Ghaza. Makumi ya wengine wamejeruhiwa.



Habari zinasema kuwa zaidi ya Wapalestina 150 wameuawa shahidi katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Ghaza katika mashambulizi ya jana ya jeshi za Israel. Jeshi la Israel linashambulia kwa makombora taasisi za kiraia na kijamii kama shule na vituo vya elimu, misikiti na makanisa, hospitali, vituo vya umeme na maji na kadhalika.


Gaza On Fire
Ni wiki tatu sasa ambapo wakazi wa Ghaza wanakabiliwa na mashambulizi makali ya nchi kavu, baharini na angani ya jeshi la Israel ambalo halikuwaonea huruma hata watoto wadogo, wanawake wajawazito, wazee na vikongwe. 

Ndege za kivita za Israel na walenga shabaha wa utawala huo ghasibu wamekuwa wakiwashambulia watoto wadogo wa Palestina wanaoonekana wakicheza mitaani. Matukio haya, kama yanavyosisitisza mashirika ya kutetea haki za binadamu, ni kielelezo cha jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu. 

Hadi kufikia leo Wapalestina karibu 1290 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 7115 wamejeruhiwa katika siku 23 za mashambulizi ya kinyama ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.

Raia wa Ghaza ambao wako katika mzingiro wa pande zote wa Israel kwa kipindi cha miaka saba sasa wanakabiliana na utawala huo katili kwa kila walichonacho huku silaha ya watoto wadogo na wanawake ikiwa ni machozi na mayowe. Maeneo yote ya Ghaza yamejaa damu za mashahidi wanaouawa huku karibu kila nyumba ikiwa katika maombolezo ya ndugu, jamaa au rafiki.


Jambo la kusikitisha zaidi kuhusu matukio ya sasa ya Ghaza ni kimya cha jamii ya kimataifa hususan nchi za Ulaya na Marekani ambazo zimekuwa zikijigamba kuwa wabeba bendera ya kutetea haki za binadamu. Nchi za Magharibi hazikuishia katika kunyamaza kimya mbele ya mauaji hayo ya kutisha yanayofanywa na utawala katili wa Israel huko katika Ukanda wa Ghaza, bali zinausaidia utawala huo wa kigaidi kwa silaha zaidi. Kwa kweli yanayotokea Ghaza ni maafa makubwa ya binadamu ambayo doa lake jeusi litabakia milele katika uso wa historia ya mwanadamu.


Ghaza ya leo ni mtihani mgumu kwa Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama, taasisi za kimataifa na nchi zote zinazodai kutetea haki za binadamu zinazoendelea kunyamaza kimya na kushuhudia kwa macho tu jinsi watu wa Ghaza wanavyochinjwa na mashine ya vita ya Israel.


Katika mazingira hayo linajitokeza swali kwamba je, raia wa Ghaza si wanadamu kama wengine wanaopaswa kudhaminiwa usalama na amani? Je, ni jumuiya na taasisi gani zinazopaswa kuwadhaminia usalama na amani? Ni nini majukumu ya wajibu wa Umoja wa Mataifa la Baraza lake la Usalama katika hali ya sasa ambapo watoto wadogo wasio na dhambi na wanawake wa Ghaza wanaendelea kuchinjwa na kuuawa kama wadudu wasio na thamani?  


Wednesday, July 30, 2014

Hatimaye Mkenya Wa Pili Atua Ligi Kuu England.... Atashiriki Michuano Mikubwa Ya UEFA

Divork Origi Na Sakfu Ya Liverpool.

London: Hatimaye, klabu ya Liverpool imemsajili mshambuliaji wa chipukizi, Divock Origi Mkenya/Mbelgiji akitokea Klabu yake ya Lille aliyojiunga nayo akiwa na miaka 15.

Mchezaji huyo mwenye miaka 19 ameukubali mkataba wa miaka mitano lakini ataendelea kubaki kwenye klabu yake huko Ufaransa kwa mkopo katika msimu ujao kabla ya kuhamia Anfield mwaka ujao 2015.

“Ninayo furaha kwa klabu kubwa kama Liverpool imenisajili,” Origi alisema.
Origi alicheza mechi zote tano za Ubegiji katika fainali za Kombe la Dunia la mwaka huu wakati wakipigana kuelekea robo-fainali na kuifungia timu yake bao dhidi ya Urusi.
Mbali na Origi, Liverpool pia imewanunua Rickie Lambert, 32, akitokea Southamptom na kiungo wa wa kati Adam Lallana, 25,  kutoka Southampton.
Kadhalika imewanasa Emre Can, 20 akitokea Bayer Leverkusen na winga Lazar Markovic, 20, akitokea Benfica.
Mlinzi Dejan Lovren, 25 akitokea Southamptom pia amehamia Anfield.
“Najua hii ni klabu yenye historia kubwa, wachezaji wakubwa  na mashabiki wengi,” aliongeza.
“Kwangu Liverpoool ni moja ya vilabu bora kabisa duniani na ninayo furaha sana kuwa sehemu ya historia hii.
Origi ambaye asili yake ni Kenya alianzia katika klabu ya Genk alichochezea babake, Mike Okoth kabla ya kuhamia Lille.


TETESI ZA SOKA ULAYA

Beki was Aston Villa Ron Vlaar, 29, atakuwa
 na mazungumzo na meneja wake Paul Lambert kuhusiana na hatma yake licha ya Southampton kumwania (Daily Mirror), QPR wanafikiria kumchukua kiungo wa Colombia Carlos Sanchez, 28, kwa pauni milioni 4 kutoka Elche (Daily Mirror), West Ham na QPR wamepanda dau kwa Marseille kumchukua Matheiu Valbuena baada ya kiungo huyo Mfaransa kukataa kuhamia Dynamo Moscow (L'Equipe), Manchester United na Barcelona bado wanamfuatilia Juan Cuadrado, 26, wa Fiorentina lakini huenda wakatishwa na bei ya pauni milioni, 32, ya kiungo huyo kutoka Colombia (Marca), Manchester United wamefikia makubaliano "ya mdomo" na kiungo wa Juventus Arturo Vidal, 27, ya uhamisho wa pauni milioni 47 (Tuttosport), matumaini ya Manchester City kumsajili beki kutoka Morocco Mehdi Benatia, 27, yamefifia baada ya Roma kusema hakuna dalili za mchezaji huyo kuondoka (Le Figaro), meneja mpya wa Manchester United amewaonya mashabiki wake kuwa timu hiyo huenda ikasuasua katika miezi mitatu ya mwanzo wa msimu wakati wachezaji wakianza kuzoea mbinu zake (Times), Van Gaal amesema iwapo watashinda Ligi Kuu msimu ujao na kuwapiku majirani zao Manchester City, utakuwa ushindi "mtamu" zaidi (Manchester Evening News), kiungo wa Manchester City Yaya Toure, 31, amesema huenda akasalia katika timu hiyo hadi atakapoacha kucheza soka (Guardian), mshambuliaji mpya wa Barcelona Luis Suarez, 27, ambaye anatumikia adhabu ya miezi minne, amehamia katika mji wa Pyrenees kuanza mazoezi ya msimu mpya akiwa na mwalimu binafsi (Daily Mail), Didier Drogba, 36, amesema Diego Costa, 25, atakuwa mchezaji "mkali" katika Ligi Kuu ya England (Sun), AC Milan wanafanya mazungumzo wa mshambuliaji kutoka Brazil Robinho, 30 (Le Figaro), kiungo wa Arsenal Santi Cazorla,29, bado anasakwa na Atlètico Madrid. Atlètico pia wanamfuatilia Fernando Torres, 30, na winga wa PSV Eindhoven Zakaria Bakkali, 18 (AS.com), kiungo anayefuatiliwa na Liverpool, Xeridan Shaqiri, 22, huenda akaamua kubakia na klabu yake ya Bayern Munich (Tuttosport), Borussia Dortmund na Schalke wanamtaka mshambuliaji kutoka Serbia, Aden Ljajic, 22, kutoka AS Roma (Bild), Barcelona wametangaza kumsajili kiungo kutoka Brazil, Alex Varoneze Dione anayejulikana kama "Betri" kwa miaka mitatu (Mundodeportivo), Manchester United wameanza tena kumfuatilia beki wa kati wa Atletico Madrid Miranda, baada ya Atlètico kusema wapo tayari kupokea dau la pauni milioni 23 (Metro), AC Milan wanamtaka winga wa Newcastle Hatem Ben Arfa na huenda akauzwa kwa pauni milioni 12 (Daily Star), Bayern Munich wapo tayari kusubiri hadi Oktoba kumsajili kipa wa zamani wa Barcelona Victor Valdez ambaye anauguza jeraha la goti, ingawa anaweza kusita kwenda kugombea namba na Manuel Neuer (Mundo Deportivo), QPR wanataka kumchukua Ronaldinho ambaye amemaliza mkataba wake na Atletico Mineiro (Globoesporte) na Chelsea wanakataa kutengeneza jezi zenye jina la kipa Thibaut Courtois, 22 na Romelu Lukaku, 22, kwa sababu wachezaji hao bado hawajapewa namba (Daily Star).

SHUJAA ALIYEAMBUKIZWA UKIMWI KULIPWA KSH MILLIONI 653........

Mwathiriwa mmoja wa bomu la 1998 atapata Sh652.5 milioni kama fidia baada ya kuambukizwa virusi vya HIV akijaribu kuwaokoa manusura katika shambulizi hilo la kigaidi.

William Maina alikuwa akichokoa vifusi vya jengo la Ubalozi wa Amerika, ambalo liliharibiwa kabisa na shambulizi hilo.


Alishuhudia mbele ya mahakama moja ya Amerika kwamba alikuwa akifanya kazi kando na ubalozi huo wakati wa shambulizi, na alikimbia eneo la mkasa kusaidia katika juhudi za uokoaji.
Ni katika shughuli hizo za kuwasaidia wahasiriwa ambapo alipata majeraha na mikwaruzo iliyofanya damu yake kuchanganyika na ya wahasiriwa.
Bw Maina baadaye alipatikana kuwa na virusi vya HIV ambavyo husababisha ugonjwa wa Ukimwi. Alitoa ushahidi mahakamani kuonyesha hakupata ugonjwa huo kwingine.
“Ingawa alikuwa na majeraha madogo tu ya kimwili wakati wa juhudi za uokoaji, HIV ni ugonjwa sugu, hatari na wenye kusababishia mtu fedheha unaohitaji matibabu ya maisha,” Jaji wa Amerika John Bates alisema katika uamuzi wake.
Mwathiriwa mwengine Jael Oyoo pia alifidiwa. Bi Oyoo alitolewa kwenye vifusi na waokoaji na alipata majeraha mabaya ya moto usoni na kichwani. Waokoaji walidhania alikuwa amefariki.
Kadhalika, alipoteza uwezo wa kuona katika jicho lake la kushoto na kuathiri mno kuona katika jicho la kulia. Alikuwa hospitalini kwa miaka miwili.
Wawili hao ni miongoni mwa waathiriwa wa shambulizi hilo la bomu dhidi ya ubalozi wa Amerika mjini Nairobi, waliofidiwa baada ya kupata majeraha mabaya.
Waliopoteza waume au wake zao watapata kiasi cha hadi Sh696 milioni. Wengine watapewa Sh609 milioni.

Katika uamuzi wake, Bw Bates alitoa Sh435 milioni kwa waathiriwa wa majeraha mabaya ya kimwili, kwa mfano kuvunjika sehemu za mwili, maumivu ya nyama na makovu pamoja na waaathiriwa wa kisaikolojia.

Iwapo uchungu wa kimwili na kisaikolojia ni mwingi sana – kama waathiriwa waliopata majeraha mengi na mabaya na waliopoteza uwezo wa kuona na kusikia ama waliodhaniwa kuwa wamefariki – mahakama imetoa hadi dola milioni saba (Sh609 milioni) na zaidi,” Bw Bates alisema katika kesi iliyowasilishwa na Milly Mikali na wengine.
Walikuwa wameshtaki Jamhuri ya Sudan kwa shambulizi hilo la kigaidi.
Lakini kwa waliopoteza wake au waume zao, Jaji alisema watapewa Sh696 milioni kama fidia ya wapenzi wao waliopoteza maisha.
Aidha, kwa waathiriwa waliopata majeraha ya kiakili kuandamana na majeraha madogo ya kimwili, Jaji aliamua watalipwa kati ya Sh130 milioni na Sh261 milioni. Kwa waliokuwa na majeraha kwa saa kadha, watapata fidia ya Sh87 milioni.
Iwapo kipindi cha maumivu ni kidogo atapata pesa kidogo. Kwa mfano, aeleza jaji, waliokuwa na majeraha kwa dakika 10 watapata Sh43 milioni.

Source Taifa Leo

Friday, July 25, 2014

Viongozi Wa Sasa Bavicha Hawana Sifa Tena Ya Kugombea.

Dar es Salaam. 
John Heche Mwenyekiti Bavicha Taifa 
Viongozi wote wa juu wa sasa wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) hawatagombea nafasi yoyote katika baraza hilo kutokana na umri wao kuzidi miaka 30.
Kwa mujibu wa katiba ya Bavicha, mgombea wa nafasi yoyote anatakiwa asiwe na umri wa zaidi ya miaka 30.
Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema jana kuwa yeye, Katibu Mkuu wake, Deogratius Munishi na Naibu Katibu Mkuu, Ester Daffi hawatagombea nafasi yoyote kutokana na umri walionao... “Hii ina maana kuwa baada ya uchaguzi, tutaachia madaraka na kuendelea na shughuli nyingine za chama.”
Alisema ili kuepuka udanganyifu hususan wa umri miongoni mwa wagombea wengine katika nafasi mbalimbali za baraza hilo, watahakikisha wanasimamia suala hilo kwa umakini mkubwa.
Heche alisema uchaguzi wa Bavicha katika ngazi ya taifa utafanyika Septemba 10, mwaka huu na fomu zitaanza kutolewa kuanzia Agosti 10 hadi 25 mwaka huu.
Alisema nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huo ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti bara na Zanzibar na katibu mkuu.
Nyingine ni naibu katibu mkuu bara na Zanzibar, mratibu mhamasishaji taifa, mweka hazina na wajumbe watano wa kuwakilisha kwenye baraza kuu la chama na wajumbe 20 wa  kuwakilisha vijana kwenye mkutano kuu wa chama hicho.
Rushwa
Akizungumzia suala la rushwa katika uchaguzi, Heche alisema uongozi unaomaliza muda wake umejipanga kudhibiti vitendo hivyo ili kuzuia wasaliti kujipenyeza.
Alisema kuna baadhi ya watu wamejipanga kutoa rushwa ndani ya baraza hilo ili kushinda nafasi mbalimbali kwa lengo la kuivuruga Chadema baadaye na kuidhoofisha.
Alisema chama hicho kitawawinda wagombea hao na kuwafisha katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili wachukuliwe hatua za kisheria na baadaye kufutwa uanachama.
Mwaka 2011, Bavicha ilifanya uchaguzi ambao ulitawaliwa na mizengwe na vurugu hadi kusababisha kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea.
Mwananchi Source

Tuesday, July 22, 2014

Saratani Ya Koo Na Tumbo Husababishwa Na Pombe Za Kienyeji Kama Busaa.

Wazee wakifurahia Busaa Picha kwa Hisani Ya Nation Mediu Group
Wanasayansi wameitaka kuangazia unywaji busaa wakisema unachangia pakubwa ongezeko la visa vya saratani ya koo.
Ripoti hiyo inasema ingawa kinywaji hicho ni maarufu sana hapa nchini katika jamii mbalimbali utumiaji wa mahindi, mawele na mtama au mhogo ulioharibika kutengeneza busaa unachangia pakubwa katika kuwapa sumu wanywaji ambao mwishowe hupata magonjwa mbalimbali ukiwemo saratani ya tumbo na koo.

Wanasayasi watatu kutoka Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Jomo Kenyatta(JKUAT), mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Chiba kule Japan na mwingine kutoka Kituo cha Utafiti wa Maswala ya Afya (KEMRI) wanasema udadisi umeonyesha kemikali zinazochangia usambazaji wa saratani zinapatikana katika pombe iliyonunuliwa katika vituo mbali mbali vya vileo kule Bomet.
Wadadisi waligundua kuwa wagema wana mazoea ya kutumia mahindi yaliyooza ambayo huuzwa kwa bei ya chini na wauzaji na hivyo kufanya wanywaji pombe kupata sumu iliyo ya hali ya juu.
“Kuna haja ya kutumia mahindi masafi na bidhaa nyingine katika kutengeneza pombe lakini mambo yalivyo, tunaona wagema wakipendelea kutumia mahindi yaliyooza na kutengeneza busaa ambayo baadaye hupewa wanywaji katika sherehe za mazishi, harusi, ulipaji mahari na wakati wa kutahiriwa kwa wavulana,” ikasema ripoti hiyo.
“Kemikali hizi humfanya mnywaji kupoteza uzito, kutapika mara kwa mara na pia kuhara. Lakini baada ya muda mrefu, mwili hupoteza uwezo wake wa kuzuia magonjwa na mtu akapata saratani ya koo au matumbo,” ikasema ripoti hiyo.

Hali ya wabugiaji pombe huwa mbaya zaidi kwani wao hunywa hapa na kisha kunywa pale na hii inawafanya kuwa hatarini ya kunywa sumu aina mbalimbali na hivyo kuhatarisha maisha yao zaidi.
Inaonya kuwa wagema wengine sasa wameanza kutumia chakula ya mifugo ambacho kina sumu kali na hivyo kufanya wanywaji kunywa mvinyo wenye sumu aina mbali mbali.
Wanasayansi hao, Mary Kirui, Amos Alakonya na Keith Talam-wote kutoka Chuo cha JKUAT ,Bi Christine Bii(KEMRI) na Gonoi Tohru wa Chiba wanaamini kuna haja ya serikali kuangalia ubora wa Busaa mara kwa mara ili kuinua hali ya wabobeaji pombe.

Mourinho Anena Juu Ya Ujio Wa Van Gaal Manchester United. Amwambia............



Kushoto Ni Jose Mourinho akimtania Kocha Man U Van Gaal Kulia.
Kocha wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho, amejitanua kifua kwamba hamwogopi  mkufunzi mpya wa Manchester United, Louis Van Gaal wakati msimu mpya unapozidi kukaribia kuanza.
Wawili hao ambao ni marafiki wakubwa waliwahi kufanya kazi pamoja katika klabu ya Barcelona, Mourinho akiwa mkalimani na mwenzake kocha.

Makocha hawa wawili wana mafanikio makubwa kwenye taaluma yao ya ukufunzi  japo hawajawahi kujipata katika ushindani zaidi ya mwaka wa 2010 walipokutana kwenye fainali ya dimba la klabu bingwa Ulaya.
Wakati huo Mourinho alikuwa akiifunza Inter Milan ya Italia naye Van Gaal akinoa Bayern Munich ya Ujerumani. Timu hizo zilikutana kwenye fainali hizo na  Mourinho akaibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa.
Mwaka huu, watagongana vichwa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza ambapo Van Gaal ameapa kujaribu kushinda taji katika msimu wake wa kwanza akiwa uongozini huku naye mwenzake akisisitiza wazo sawa na hilo.
“Sina wasiwasi kwamba kwa sasa yupo hapa. Mwanzo ninatamani sana kukutana na United na wala sioni cha kunipa hofu. Hii ni kwa sababu sisi sote ni makocha wazuri na ninachojua ni kuwa ataisaidi Manchester United,” Mourinho alisema.
“Van Gaal kwa mtazamo wangu ndiye aliyekuwa kocha bora wa dimba la dunia na ni mtu ninayemheshimu sana kutokana na urafiki wetu mkubwa wa siku nyingi. Ila pamoja na yote, katika ushindani kila mmoja atajisimamia,” aliongeza.
Van Gaal alianza majukumu yake mapya klabuni humo juma lililopita na tayari ameapa kuirejesha United kwenye hadhi yake ya ushindani ligini baada ya kumaliza ya saba msimu uliopita chini ya ualimu wa David Moyes aliyepigwa kalamu.
Kwa sasa Van Gaal yuko na kikosi hicho jijini Miami, Marekani anakokitayarisha kwa mechi kadhaa za kirafiki. Kwa wakati huo huo anaendelea kufanya usajili ili kukirutubisha kikosi hicho hata zaidi.

Mkataba Wa Vana Gaal
Mkufunzi huyo alitia saini kandarasi ya miaka mitatu na United na mechi yake ya kwanza ya Ligi inayoanza Agosti 16, itakuwa dhidi ya Swansea siku mbili kabla ya Chelsea kuanza kampeni yao vile vile dhidi ya Burnley iliyopandishwa daraja.
Tetesi Za Usajili
Boss wa Manchester City Manuel Pellegrini anapanga kumchukua Didier Drogba, 36, ambaye pia anasakwa na klabu yake ya zamani Chelsea (Daily Star), meneja wa Manchester United Louis van Gaal anataka kutoa pauni milioni 17 kumchukua beki mkabaji wa Ajax Daley Blind, 24 (Daily Express), United pia wameripotiwa kuwa karibu kumsajili beki wa kati wa Borussia Dortmund Mats Hummels, 25, kwa pauni milioni 16 (Daily Mail), Tottenham wameambiwa watoe pauni milioni 25 kama wanamtaka kiungo wa Real Sociedad Antoine Griezmann, 23, ambaye pia anafuatiliwa na Chelsea na Monaco (Daily Telegraph), boss wa Arsenal, Arsene Wenger amesema hatosajili mshambuliaji msimu huu na hivyo kufuta tetesi zinazomhusisha na Mario Balotelli wa AC Milan (Daily Mirror), kiungo wa Ureno Thiago Mendes, 23, ametupilia mbali uwezekano wa kurejea Chelsea na angependa kusalia Atletico Madrid miaka miaka mingine miwili (Daily Express), PSG watakwepa sheria za Fifa za fedha kwa kumchukua Angel Di Maria, kwa mkopo kwa mwaka mmoja kutoka Real Madrid. Di Maria anasakwa pia na Man United (Daily Express), Arsenal, Chelsea na Man United wanamtaka beki Reece Oxford, 15, baada ya kinda huyo kuonesha kipaji msimu uliopita akiwa na West Ham ya vijana (Daily Star), Arsene Wenger atamruhusu Thomas Vermaelen kwenda Manchester United, ikiwa tu atarhusiwa kumchukua Phil Jones au Chris Smalling (Daily Mirror), Chelsea watampa Didier Drogba mkataba wa miezi 12 wa kucheza ambao hautakuwa na kipengele cha kuwa kocha, ingawa Chelsea wapo tayari kuzungumzia hilo (Daily Telegraph), mshambuliaji wa Lille Divock Origi anakwenda Boston Marekani kuungana na Liverpool ambao wapo katika ziara ya mechi za kabla ya msimu. Atafanyika vipimo kabla ya kukamilisha uhamisho wake wa pauni milioni 10. Huenda pia akarejeshwa Lille kwa mkopo (Daily Star).



Monday, July 21, 2014

Mkenya Aliyecheza World Cup Kutua Liverpool

Liverpool inakaribia kufikia maafikiano na klabu za Southampton kumnunua beki Dejan Lovren na klabu ya Lille ili kupata saini ya mshambuliaji Mkenya Divock Origi.
Divorck Origi

Kulinganana BBC, The Reds ambao kwa wakati huu wako ziarani nchini Marekani wameripotiwa kufikia makubaliano na Lille kumsajili Origi raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Kenya kwa dau la Sh1.5 bilioni. Kwa wiki kadhaa sasa Liverpool imekuwa ikimsaka mshambuliaji huyo huku kukichapishwa ripoti kadhaa za maafikiano baina ya pande zote ila taarifa hizo hazijawahi kuwa rasmi.
Kumhusu mlinzi Lovren mwenye umri wa miaka 25, Liverpool waliwasilisha ofa ya Sh3 bilioni juma lililopita ila ilikakataliwa. Hata hivyo Lovren raia wa Croatia ameelezea nia yake ya kutaka kuhamia Liverpool hatua ambayo imeanza kuwafanya Southampton kuwaza mara mbili.
Mlinzi huyo amewasilisha barua kwa klabu hiyo ya kuwataka wamruhusu aondoke ikiwa ni baada ya kutumikia mwaka mmoja wa mkataba wake wa miaka minne nao.
Liverpool ambao watashiriki Ligi ya mabingwa msimu ujao kwa mara ya kwanza tangu 2009, wamekuwa wakikirutubisha kikosi chao na hadi kufikia sasa baada ya kuondoka kwa nyota wao Luis Suarez aliyetua Barcelona, wamefanikiwa kuwasajili wachezaji sita.

Mshambuliaji Loic Remy alijiunga nao Jumapili baada ya klbu ya QPR kukubali ofa yao ya Sh1.2 bilioni. Kando na mchezaji huyo, kocha Berndan Rodger ameanunua Adam Lallan, Rickie Lambert, Lazar Markovic na Emre Can...

Kwa tetezi nyingi za soka usikose kujiunga nasi kila mara....

Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score